Siri imekuwa siri, na si siri tu, bali ni kilinge; yaani kunga. Matesa ametekwa na
kufanywa mfungwa. Swali ni: Je, mwanadamu akumbanapo na masuala
magumu kama vile amani, uonevu, watawala dhalimu, mapenzi changamano,
afanyeje?
Atakayemwokoa mwenye kuteseka hajulikani; ni Kidhabi ama ni Mwanalemba?
Ni kitu gani kilichomfanya mtetezi kufanywa mhanga; mwinda kuwa
mwindwa?
Kwa hali yoyote ile, Siri Sirini ni fumbo pevu; lakini upo mwanya mmoja wenye
kutufumbulia fumbo lenyewe. Mwanya wenyewe umo kwenye mshororo
mmoja baina ya mingine katika shairi; mshororo ulio chama siri kali. Je, siri hii
ni siri gani yenye kula vichwa vya wajinga na weledi? Haitanzuki siri, imetanza
mba; imekukutaa na ukakamavu! Vikao vya kumfuma "msaliti," vimeshamiri,
vilinge vimekolea, urazini umepotea. Siri, imo sirini! Ni siri gani hii jamani?
Siri Sirini: Mshairi na Mfungwa ni riwaya ya kwanza katika msururu wa riwaya
tatu zenye ku kirisha, kuhifadhi historia kama tarikhi huku masuala ya utawala
wa kisiasa na utendajikazi unaotarajiwa katika muktadha huo ukichimuza. Ni
riwaya inayosheheni uchangamfu na karipio kwa wakati mmoja. Usomapo
riwaya hii ya kwanza, utajikuta umepata hamu kuu ya kuipata ya pili nayo
uisome bila kuchelewa; na ukiisoma ya pili, basi hutakuwa na budi bali kuisaka
na kuisoma ya tatu vile vile.
Rocha Muzungu Chimerah ni mwandishi wa riwaya mwenye tajiriba na kipawa
cha aina yake. Anatumia mtindo wa kuchangamsha moto mmoja katika
uandishi wake huku akiangazia masuala mazito ambayo wengi hushindwa
kupata ujasiri wa kuyaandikia. Ukweli katika mambo yamshughulishayo katika
msururu huu wa riwaya ni kama kijembe cha sumu, lakini anavyousema ukweli
huo ni kama uki wa nyuki, unaokuacha ukijirambaramba mdomo kitambo
kizima baada ya kuumeza uki huo.