Mwanamke kama dutu la udongo wa mfinyanzi huumbwa na kuumbuliwa
na jamii kwa namna mbalimbali. Kama kinyonga, uso wake unabeba rangi
tofauti tofauti kulingana na mikondo ya maisha na mapigo ya wakati.
Itakuwaje mwanamke awe wa kuozwa kama mwenye ugaga wa hisia za
kujichagulia mwenyewe; au awe wa kuuzwa kama pakacha la maembe
katika soko la umma? Uso wa mwanamke ni njia mbilimbili; ikiwa hazai
analea, asipokuwa akirembesha anarembeshwa, kama hatumbuizi
anatumbuizwa, ikiwa hajengi anabomoa; na kila mtu anamtazama na
kumtarajia aonyeshe uongofu wa malaika kama kwamba yeye si mtu.
Haya yanapokolea ndipo mwanamke anaonyesha nyuso zake.
Nana, msichana mrembo anajipata katikati ya jamii yenye mielekeo ya
kumfinyanga mwanamke na kumyumbisha kama kayamba. Kila
anayemwona Nana anamchukulia kuwa ni pambo la mji lenye nyuso
nyingi au lisilokuwa na uso hata mmoja. "...Bwana Hila... alidhani tu
maisha ya mwanamke ni kustareheshwa ...anachostahiki ni kupewa kila
kitu anachokitaka...apewe mawazi ya kifahari, manukato ghali, chakula
cha rutuba...mradi tu mwanamke abaki ndani kungoja kumstarehesha
bwana."
Anapotambua kuwa ana nyuso nyingi, Nana anajitazama kwa kioo kipya
na kuanza safari mpya.